Ijumaa 20 Novemba 2026 - 12:03
Hukumu za kifungo cha maisha kwa wanazuoni; Mkakati mpya wa utawala wa Bahrain wa kutekeleza utawala wake na ukandamizaji wa kidini

Hawza/ Kufuatia kutolewa hukumu kali za kifungo cha maisha na vifungo vingine vya gerezani dhidi ya wanaharakati 69 wa kiraia na wanazuoni mashuhuri wa Kishia nchini Bahrain, Harakati za Mapinduzi za nchi hiyo, katika taarifa kali, imeelezea hatua hizo kuwa ni “onyesho la kejeli la haki” na taswira ya fikra za kulipiza kisasi za utawala uliopo madarakani.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Harakati za Mapinduzi za Bahrain, zikiendelea kufuatilia na kushiriki katika kukabiliana na hali mbaya ya kisiasa nchini humo, zinaamini kuwa kile ambacho utawala uliopo madarakani unajaribu kukilazimisha kama mfumo wa ndani kwa lengo la kufidia uhalali wake uliopotea, kinasimama juu ya misingi miwili: ukamataji wa mamlaka kwa mkono wa chuma na kutegemea nguvu za kigeni. Mambo yote mawili hayawezi kuzaa matunda mengine isipokuwa kuongeza mpasuko kati ya wananchi walio wengi na utawala. Hatimaye, mpasuko huu ni kama handaki lisilo na njia ya kurudi, linaloelekea kupotea kwa uwezekano wowote wa makubaliano na kuelekea kwenye mabadiliko ya kimsingi.

Utawala uliopo madarakani, kupitia hukumu hizi zenye misukumo ya kisiasa zilizotolewa dhidi ya wanazuoni wakubwa wa Kishia, wakiongozwa na Ayatullah Sheikh Isa Ahmad Qasim, umepiga pigo kubwa kwenye mshikamano wa kitaifa na uwezekano wowote wa makubaliano ya kisiasa. Aidha, umeimarisha ukweli wa tabia yake ya kuchukiza ya ubaguzi wa kimadhehebu na kuchagua njia ya makabiliano ya kuamua uhai na hatima badala ya kuishi pamoja na kukubali uwepo wa mwengine.

Hukumu zilizotolewa kwa pamoja ni onesho la kejeli la haki na taswira ya fikra za kulipiza kisasi za utawala uliopo madarakani

Harakati za Mapinduzi, kwa kuzingatia hali ya ndani iliyochanganyikiwa kisiasa na mazingira ya kikanda yaliyo katika hatari ya kulipuka, zinatangaza msimamo wake katika mihimili kadhaa muhimu kama ifuatavyo:

Kwanza: Tunasisitiza umuhimu wa tamko lililotolewa na Ayatullah Sheikh Isa Qasim tarehe 25 Aban 1405 (16 Novemba 2026), na tunasisitiza ulazima wa kutekeleza kwa vitendo yaliyomo ndani yake katika uwanja wa utekelezaji. Vilevile, tunautahadharisha utawala uliopo madarakani na kuutaka urudi kutoka katika njia yake potovu na kuacha kuweka matumaini katika misaada ya kigeni; kwa sababu utulivu hauwezekani isipokuwa kupitia makubaliano ya kisheria, na makubaliano hayo hayapo tena. Utawala uliopo madarakani, kupitia mwenendo wake, umeyapiga makubaliano hayo “risasi”.

Pili: Tunawashukuru na kuwapongeza watoto wa taifa hili kwa misimamo yao ya heshima na shughuli zao endelevu za kupinga hali iliyopo, kwa kuonesha mshikamano na wafungwa wote na kupinga hukumu za kulipiza kisasi na za kikatili zilizotolewa dhidi ya wanazuoni tarehe 25 Aban 1405 (16 Novemba 2026). Tunasisitiza ulazima wa kuendelea na maandamano na mshikamano kwa nguvu na kiwango kikubwa zaidi, kwa upande wa idadi na ubora; ikiwa ni pamoja na kudhihirisha uaminifu kwa wanazuoni na kuisaidia dini, alama za kidini na sifa za kimadhehebu ambazo leo zimekuwa uwanja wa kulengwa na kushambuliwa kidhuluma na mfumo wa utawala uliopo madarakani.

Vilevile, tunatoa shukrani zetu kwa Maraji' wote, wanazuoni, Hawza za kielimu, vyama, viongozi na wanaharakati, waliopo ndani na nje ya Bahrain, ambao wameshiriki katika kuwasaidia wanazuoni na masuala ya wananchi wa Bahrain, na tunawaomba waendelee na mshikamano huo.

Tatu: Tunakataa kulengwa na kuchafuliwa haiba ya wanawake wa Bahrain, na tunalaani kutolewa  hukumu kali na zisizo na huruma ambazo hazina chembe yoyote ya ubinadamu. Vilevile, tunahofia sana kuteswa na kuadhibiwa kwa mfungwa Badour Abdulhamid Ali, pamoja na kuthibitishwa hukumu ya kifungo cha maisha dhidi yake katika kesi isiyo ya haki, ambayo haina hata vigezo vya msingi kabisa vya haki.

Baada ya hapo, kuendelea kutumia kesi hii kwa ajili ya kuwadhihaki Mashia na kuchochea kampeni zisizodhibitiwa za tuhuma na usaliti, ambazo zinasababisha kuongezeka chuki na kuharibu muundo wa kitaifa, ni hatua zinazofanyika katika mwelekeo wa kutekeleza mipango mibaya ya utawala uliopo madarakani.

Nne: Tunafuatilia operesheni zinazoendelea za ukandamizaji katika maeneo ambayo waandamanaji wa amani hujitokeza, na tunazielezea hatua za vikosi vya usalama kuwa ni “za kinyama”; kwa sababu vinatumia adhabu za pamoja katika mfumo wa kimadhehebu unaolenga maeneo wanayoishi Mashia.

Mfumo huu wa ukandamizaji umewahi kutumika hapo awali na kusababisha ukiukwaji wa haki na uhalifu wa kutisha. Jambo hili linahitaji ulimwengu huru kusimama upande wa taifa letu lililodhulumiwa, ambalo limekuwa likilengwa na mashine ya kikatili ya ukandamizaji. Kunyamaza mbele ya hali hii hakuruhusiwi.

Mwisho, tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awafanye watoto wa taifa letu wawe imara na awasaidie. Haki yetu haitapotea kamwe, na sisi, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, tutaendelea kubeba amana yetu ya kidini na kitaifa.

Kumbukumbu ya mashahidi wenye nyoyo safi na tabia njema idumu milele, na uhuru upatikane kwa wafungwa walio huru.

Imetolewa na Harakati za Mapinduzi za Bahrain.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha